HABARI MPYA

Saturday, January 4, 2014

DAR ES SALAAM, Tanzania.


MAKAMU Mwenyekiti wa CCM, Philip Mangula amecharuka na kusema kwamba Wana-CCM ambao wameanza sasa kutangaza kugombea nafasi mbalimbali za uongozi katika uchaguzi Mkuu utakaofanyika mwakani, ni wasaliti wakubwa ndani ya Chama.

Mangula, ametoa karipio hilo, leo (jana) wakati akitoa Salamu za Mwaka Mpya wa 2014 katika mkutano wa dharura wa Kamati ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi Tawi la Ofisi Ndogo ya Makao Makuu jijini Dar es salaam.

Huku akinukuu kanuni zinalzolinda Maadili ya Uchaguzi na uteuzi wa wagombea ndani ya Chama, Mangula, alisema hadi sasa hakuna kikao chochote cha ngazi ya juu cha Chama, kilichoruhusu wanachama kuanza kutangaza nia za kugombea uchaguzi hadi pale itakapofika mwaka 2015.

Makamu huyo wa CCM (Bara), alisema, wanachama wanaojipitisha sasa kwa wananchi kwa namna moja au nyingine kwa lengo la kutangaza nia ya kuwania nafasi katika uchaguzi mkuu ujao, ilihali muda wa kufanya hivyo haujafika ni wasaliti au waasi ndani ya Chama.

Mangula alisema, wanaofanya hivyo ni waansi na wasaliti wakubwa kwa sababu wanaibua na kuendeleza makundi mapemba huku wakijua kwamba hali hiyo hukifanya chama kuwa na wakati mgumu wakati wa uchaguzi.

Kutokana na hali hiyo, amesisitiza kuwa Chama, hakipo tayari kuona au kuwavumilia watu wachache ndani ya Chama wanaoendelea kuvuruga umoja, mshikamano na misingi ya Chama kwa sababu tu ya umangimeza na uroho wa madaraka uliokiuka kiwango.

Mangula aliwataka wana-CCM na kwa jumla wakiwemo hao wa Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM, Lumumba, kuzingatia wakati wote misingi mizuri ambayo itawezesha kupatikana viongozi wazuri ambao hawatokani na mianya ya rushwa ili kuwa na dira nzuri kuelekea katika uchaguzi Mkuu utakaofanyika 2015.  CCM BLOG

No comments:

Post a Comment