Tuesday, February 19, 2013

WANACHAMA ZAIDI TAWI LA CCM NAPOLI 2013

Mwenyekiti wa tawi la Chama Cha Mapinduzi ndugu Abdulrahamani A.Alli  akiwa na Katibu uenezi na Siasa wa tawi wakati wa kumuapisha mwanachama mpya wa CCM. 

Mwenyekiti akitoa maelezo mafupi kwa mwanachama mpya wa CCM wakati wa kukabidhi kadi ya uanachama.

Katibu  mwanezi na siasa wa tawi  ndugu Allan Bendera  akisalimiana na mwanachama mpya ndugu Jeremiah  William  Maselle




Mwenyekiti wa tawi la Napoli ndugu Abdulrahamani A.Alli amewatangazia  wote waliojaza fomu za kujiunga na Chama cha Mapinduzi tawi la Napoli kuwa watafahamishwa baada ya kikao cha Halmashauri kuu ya tawi.

Wednesday, January 23, 2013

CCM KUTUMIA PIA SHEREHE ZA MIAKA 36, KUTATHMINI UCHAGUZI WAKE MKUU ULIOPITA


NA BASHIR NKOROMO, DAR ES SALAAM
PAMOJA na mambo mengine, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimepanga kuzitumia sherehe za miaka 36 ya kuzaliwa kwake, kufanya tathmini ya uchaguzi wake mkuu wa viongozi mbalimbali uliomalizika mwishoni mwa mwaka jana.

Lengo la tathmini hiyo ni kujifunza au kukumbushana kwa kina changamoto zilizojitokeza, hivyo kuitumia fursa hiyo kujipanga vizuri zaidi kwa ajili ya uchaguzi mkuu mwingine wa ndani ya Chama wa mwaka 2017.

Hayo yalisemwa na Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye alipozungumza na waandishi wa habari leo, Januari 21, 2013, katika Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM, jijini Dar es Salaam.

Nape alisema, sherehe za miaka 36 ya kuzaliwa kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM), zitafikia kilele chake Februari 3, 2013, na zitafanyika Kitaifa kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika mjini Kigoma.

Alisema, mgeni rasmi katika sherehe hizo ni Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete na zitahudhuriwa pia na Makamu Wenyeviti wa CCM (Zanzibar) Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein, Makamu Mwenyekiti wa CCM (Bara) Philip Mangula na Wajumbe wote wa Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya Taifa wakiongozwa na Katibu Mkuu, Abdulrahman Kinana.

Nape alisema, uamuzi wa kufanya kilele cha sherehe hizo kuwafanyika Februari 3, 2013 ni kutokana na tarehe yenyewe ya kuzaliwa kwa CCM, ambayo ni Februari 5, 2013 kuwa siku ya kazi, hivyo kutoweza kutoa fursa kwa wanachama kushiriki kwa ufanisi katika sherehe hizo muhimu kwao.

"Sherehe hizi za miaka 36 ya kuzaliwa kwa CCM zinafanyika ikiwa ni takriban miezi miwili tu tokea kumalizika kwa uchaguzi mkuu wa ndani ya Chama na jumuiya zake zote ukamilike Novemba 13, 2012,
Kwa hiyo ni sherehe muafaka kujipongeza na vilevile kuwashukuru wanachama wake kwa kukamilisha kwa ufanisi uchaguzi huo", alisema Nape.

Alisema ili kuwashirikisha wanachama katika ngazi zote, uzinduzi wa sherehe hizo utafanyika kwenye matawi yote, Jumatano Januari 30, 2013, kwa kufanya mikutano ya wanachama wote, nafasi ambayo itatumika kufanya tathmini ya uchaguzi mkuu wa CCM na jumuiya zake wa mwaka 2012 katika ngazi hizo.

Nape alisema Alhamisi Januari 31, 2013 itakuwa ni siku ya Umoja wa Vijana (UVCCM) ambapo wanachama wa jumuiya hiyo watashiriki katika shughuli mbalimbali za kijamii ambazo alisema ni pamoja na usafi wa mazingira na upandaji wa miti.

"Kazi nyingine zitakazofanywa na vijana ni kujadili mafanikio ya UVCCM katika kipindi cha miaka 36 tokea kuzaliwa kwa CCM na Shughuli nyingine itakuwa ni kufanya tathmini ya uchaguzi mkuu wa CCM na jumuiya zake wa mwaka 2012, na mwisho ni kufanyika kwa matamasha mbalimbali ya michezo yatakayowahusisha vijana wote". alisema Nape.

Alisema Februari Mosi, 2013, itakuwa Siku ya Umoja wa Wazazi. Hao watashiriki katika shughuli za kijamii ikiwa ni pamoja na kupanda miti, kushiriki katika ujenzi wa miradi ya maendeleo kama vile ujenzi wa madarasa, zahanati, nyumba za walimu na kadhalika.

Shughuli nyingine itakayofanywa na Wazazi ni kufanya tathmini ya uchaguzi mkuu wa CCM na jumuiya zake wa mwaka 2012, na pia watajadili mafanikio ya jumuiya hiyo yenyewe kwa miaka 36 iliyopita.
Jumamosi Februari 2, 2013 itakuwa siku ya Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT).

Nape aliendelea kueleza kwamba shughuli zitakazofanywa na wanachama hao wa UWT ni kufanya usafi, kupanda miti, kutembelea na kufariji wagonjwa katika hospitali na vituo vya afya, kutembelea vikundi vya uzalishaji mali vya kina mama, kufanya tathmini ya uchaguzi mkuu wa CCM na jumuiya zake wa mwaka 2012 na mwisho ni kujadili mafanikio ya UWT kwa miaka 36 iliyopita.

Siku ya kilele cha sherehe hizo ambazo alisema kaulimbiu yake ni Umoja ni Ushindi kutafanyika Matembezi ya Mshikamano na kwamba wanachama wa CCM na jumuiya zake zote nchini kote ambazo ni UVCCM, Wazazi na UWT watafanya Matembezi ya Mshikamano katika kila tawi kwa muda ambao kila tawi litaona unafaa kwa kuzingatia hali halisi ya mazingira ya eneo husika.

Vilevile itafanyika mikutano ya wanachama wote kwenye matawi, kata, wilaya na mikoa ambayo itatumika kupokea na kujadili maazimio ya Mkutano Mkuu wa CCM uliofanyika tarehe 11 – 13 Novemba, 2012 na utekelezaji wa Mradi wa Awamu ya Tatu wa Kuimarisha Chama.

Friday, December 28, 2012

CCM DIASPORA KATIKA MKUTANO MKUU WA NANE WA CCM 2012.

Mwenyekiti wa tawi la Chama Cha Mapinduzi CCM Napoli Italy, ndugu Abdulrahamani A.Alli katika picha na Mh. Balozi Ali Karume aliyekuwa balozi wa Tanzania Rome Italy.
Baadhi ya wajumbe wa  CCM Diaspora katika picha ya pamoja na Mama Salma Kikwete baada ya kuhudhuria mkutano mkuu wa CCM kizota.

Meya wa Tanga Mh. KISAUJI  akisalimiana na wana CCM Diaspora katika mkutano mkuu wa CCM 2012


Monday, December 3, 2012

NAPE: VIGOGO CHADEMA WANA KADI ZA CCM




*Wengine wanaendelea kuzilipia mpaka leo
*Ahoji Dk. Slaa kairudisha lini na wapi?
*Awaita waganga njaa si wanasiasa


MWANZA,TANZANIA
KATIBU wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Itikadi na Uenez Nape Nnauye, amerusha kombora kuwa vigogo wengi ndani ya CHADEMA wameendelea kuwa na kadi za CCM na wengine wanaendelea kuzilipia, jambo linalothibitisha unafiki walionao viongozi wengi wa upinzani nchini.

Akifungua mkutano wa Halmashauri Kuu ya CCM wilaya ya Nyamagana, jijini Mwanza, leo uliokuwa na lengo la kupokea maazimio ya Mkutano Mkuu wa nane wa CCM na hotuba ya Mwenyekiti wa CCM Taifa Rais Jakaya Kikwete, Nape amedai siasa kwa sasa imevamiwa na makanjanja wengi ambao kazi yao ni kuganga njaa na hivyo huishi kinafiki kwakuwa wakisemacho sicho wanachokiishi.

Sambamba na kombora hilo, Nape ameitaka CCM kuhakikisha inatoa uongozi mzuri ili kudhibiti uvamizi huu wa makanjanja kwenye siasa za hapa nchini. SOMA ZAIDI

Saturday, November 24, 2012

KINANA AZUNGUMZIA URAIS 2015

 
Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimewatisha makada wake kwa kuwaeleza kuwa kitamtosa bila kumuonea haya mwanachama yeyote atakayeomba kuteuliwa kugombea urais mwaka 2015 huku akiwa kinara wa kutegemea makundi ya kumwigiza katika nafasi hiyo.
Katibu Mkuu wa Chama hicho, Abdulrahman Kinana, alisema badala yake CCM itahakikisha mgombea inayemsimamisha ni mwanachama asiyeendekeza makundi, mwadilifu ambaye kila akiteuliwa atakuwa hatiliwi shaka.
Alitoa kauli hiyo jana wakati akijibu swali la mmoja wa wana-CCM katika mkutano wa shina la Isesa mkoani Rukwa, akiwa katika ziara ya kujitambulisha na sekretarieti mpya na kueleza usimamizi na utekelezaji wa ilani ya CCM.
Jibu hilo lilitokana na mwanachama huyo, Peter Lilata kutaka kujua CCM imejiandaa vipi kuhakikisha katika Uchaguzi Mkuu wa 2015 inateua mgombea ambaye atakubalika na wananchi wengi, na kutofanya kosa kuteua mgombea ambaye hakubaliki kwa maelezo kuwa kufanya hivyo kutakisababishia chama usumbufu katika kupata ushindi.

Kinana hakuwataja vinara wa makundi, lakini baadhi ya makada wamekuwa wakitajwa kuwa na nia ya kugombea urais mwaka 2015.
Baadhi ya wanaotajwa ni Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa; Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe; Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta na Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye. Hata hivyo, hakuna aliyewahi kuthibitisha kuwa atagombea zaidi ya kusema kuwa watafanya hivyo kuda ukifika.
Mapema akizungumza baada ya kuzindua shina hilo, Kinana aliwataka viongozi wa CCM kuonyesha mfano wa ujenzi wa Chama kwa kutembelea ngazi za mashina na matawi.
“Kuanzia sasa tutawapima viongozi wetu kwa namna wanavyokuwa wepesi kutembelea mashina na matawi ya CCM kwa sababu utaratibu huu ndiyo pekee utakaokiimarisha Chama, na si vinginevyo,” Kinana na kuongeza:
“Kutokana na kutambua hilo na kwa kuwa ni maelekezo yaliyotokana na maazimio kwenye Mkutano wetu Mkuu uliomalizika hivi karibuni mjini Dodoma, ndiyo sababu baada ya kupatiwa wadhifa huu mimi na wenzangu tumeanza ziara hii, na kila ninapofika lazima nitembelee mashina na matawi ili kuwa mfano kwa viongozi wengine.”
Akizungumzia rushwa na mizengwe katika uchaguzi, aliwataka wana-CCM kuhakikisha kuwa katika kila chaguzi wanahangaika kuunga mkono wagombea ambao ni watendaji wazuri na wenye maadili safi badala ya kukumbatia wanaowapa rushwa.
“Lazima mjue kwamba mnapoamua kumchagua mgombea anayewapa rushwa, mnafanya kosa kubwa sana kwenu, maana akishapita anakuwa kiongozi wa kutetea maslahi yake na siyo yenu,” alisema Kinana.
Aliwataka wana-CCm kuacha kutungiana fitina, mizengwe na kuacha makundi kila baada ya chaguzi kwa sababu mambo hayo yanachangia kwa kiasi kikubwa kudhoofisha mshikamano na umoja ndani ya Chama.
Aidha, Kinana amewahakikishia Watanzania, hususani wanachama wana-CCM kwamba yupo tayari kuhakikisha anatekeleza kwa ufanisi mkubwa majukumun makubwa aliyopewa.
“Ni kweli nilikuwa nimetangaza kustaafu siasa kwa kuzingatia kwamba nimeshashika kwa muda mrefu nyadhifa za kuchaguliwa, nikaona kwamba kama wenzako wameshakuamini mwa muda mrefu ukafanya nao kazi wakikupenda, basi usisubiri mapaka uchokwe ndiyo uondoke,” alisema na kuongeza.
“Lakini sasa baada ya maamuzi yangu, Mwenyekiti wa Chama Chetu, Rais Jakaya Kikwete akaamua kwa kadiri alivyoona inafaa, akaniteua nikisaidie Chama. Kwa mtu mwenye hekima na uadilifu unapoteuliwa na Mwenyekiti wa Chama chako, tena Rais wa Chama kinachotawala, lazima ukubali tena bila kinyongo, nikakubali.”
“Sasa baada ya kuwa mimi ndiye Katibu Mkuu wa Chama hiki, napenda kuwaambia kwa dhadi ya moyo wangu kwamba nipo tayari, kimwili, kiakili kuhakikisha nawatumikia Wana-CCM na watanzania kwa jumla kwa weledi na ufanisi mkubwa,” alisema.
Kinana anafuatana na Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (Nec) Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye na Katibu wa Oganaizesheni, Mohamed Seif Khatib na baadhi ya mawaziri.
‘TUITANE NDUGU’
Katika hatua nyingine, Kinana ameagiza kuanzia sasa wanachama wa CCM kuacha kuitana waheshimiwa badala wake watumie jina la ndugu kama alivyoasisi Mwenyekiti wa kwanza wa CCM, Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere.
“Katika maisha yangu yote ya kumfahamu Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Nyerere, sikupata kumsikia akijiita au akitaka aitwe Mheshimiwa Mwenyekiti, au Mheshimiwa Rais, sasa haya mambo ya sisi kuitama mheshimiwa tunayatoa wapi?” alihoji Kinana.
Alisema, Mwalimu Nyerere hakujiita mheshimiwa kwa sababu ina maana kubwa sana, kwa hiyo ni lazima Wana-CCM kuendelea utamaduni huo wa kuitaka ndugu kwa sababu unazuia matabaka ya ubwana na utwana.

Wednesday, November 14, 2012

RAIS KIKWETE ATANGAZA SEKRETARIETI MPYA YA CCM

Abdulrahman Kinana-Katibu Mkuu wa CCM, Taifa
Kwa habari zaidi za Mkutano mkuu wa nane wa CCM 2012  click hapa

Tuesday, November 13, 2012

DIASPORA WAKIWA KIZOTA

WANA CCM DIASPORA KATIKA PICHA YA PAMOJA NA VIONGOZI WAKUU WA CHAMA CHA MAPINDUZI KATIKA MKUTANO MKUU WA NANE WA CCM 2012

Saturday, November 10, 2012

Monday, November 5, 2012

MODENA ITALY:SHINA JIPYA LA CCM

CCM YASONGA MBELE ITALY!
 
Mwenyekiti wa shina Bi Mary Julius Mtemahanji katika picha ya pamoja na viongozi wa Tawi la CCM la Napoli Italy mara baada ya kuchaguliwa na wanachama wa CCM Modena katika ufunguzi wa shina la kwanza Italy.
 


 Bi Salama Kasiba akiangalia skafu ya CCM akiwa na katibu uchumi na Fedha wa tawi la CCM Napoli, ndugu FATUMA A.TANDIKA.
Pichani ni Mzee PASKAL NYALUS JONAS  (mjumbe) akiwa na Bi ESTHER EVAREST NGINGU (mjumbe)



Katibu wa Tawi la CCM la Napoli ndugu KAGUTTA NSANGU MAULIDI akitoa hotuba kufafanua katiba ya chama juu ya utaratibu wa shina na taratibu za uchaguzi. Pamoja nae katikati ni Mwenyekiti wa Tawi la CCM la Napoli Ndugu ABDULRAHAMAN A. ALLI na Katibu wa uchumi na fedha ndugu FATUMA A.TANDIKA

Tarehe 3/11/2012 itabaki katika  historia ya Chama cha Mapinduzi ughaibuni , baada ya kufunguliwa shina la kwanza nchini Italy. Ufunguzi huo ulisimamiwa na kuendeshwa na viongozi wa Tawi la Napoli ambalo ni tawi pekee nchini Italy.Wanachama wa CCM Modena  walimchagua Bi MARY  JULIUS MTEMAHANJI kuwa Mwenyekiti, baada ya mchuano mkali wa kura kati yake na ndugu PASKAL NYALUSI JONAS ambaye baadae alichaguliwa kuwa mjumbe wa kamati ya uongozi. Wengine waliochaguliwa ni Katibu wa shina ndugu MWINYIMWAKA HATIBU SARAI, bi HALIMA MWEVI, Bi SALAMA KASIBA, na Bi LEYLA  RAYMOND walichaguli kama wajumbe wa kamati ya uongozi.

Saturday, October 20, 2012

UCHAGUZI MKUU CCM

Katibu wa NEC,Itikadi na Uenezi ,Nape Nnauye akiongea na waandishi wa habari,ofisi ndogo za CCM
Lumumba Dar es salaam.
MKUTANO MKUU WA CCM 2012

Kikao cha Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa kilichofanyika tarehe 13/10/2012 pamoja na mambo mengine kilipanga ratiba ya Mkutano Mkuu wa Taifa iwe kama ifuatavyo:-

Mkutano Mkuu wa Nane wa Kawaida wa CCM utafanyika tarehe 10 – 12 Novemba, 2012 . Kwa kawaida Mikutano Mikuu ya CCM imekuwa ikifanyika kwa siku mbili. Lakini safari hii CCM imeamua mkutano huo uwe wa siku tatu ili kutoa fursa kwa Wajumbe kujadili kwa kina taarifa muhimu zitakazowasilishwa.

Mkutano huo utafanyikia KIZOTA – Dodomamahali ulipofanyika Mkutano Mkuu uliopita mwaka 2010.

Shughuli muhimu zitakazofanywa wakati wa Mkutano huo zitakuwa:-

Kufanya marekebisho ya Katiba ya CCM ya 1977 toleo la 2010 kwa kuzingatia mapendekezo ya Halmashauri Kuu ya Taifa yatakayowasilishwa kwenye Mkutano huo.

Kupokea na kujadili taarifa mbalimbali zikihusu:-

Taarifa ya Kazi za Chama kwa Kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2007-2012 itakayowasilishwa na Halmashauri Kuu ya Taifa.

Taarifa ya Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010 ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Shughuli za Uchaguzi ambazo zitahusu Uchaguzi wa:-

Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa Viti Kumi vya Bara na kumi vya Zanzibar.

Mwenyekiti wa CCM.

Makamu wawili wa Mwenyekiti mmoja kutoka Bara na mwingine kutoka Zanzibar.

Shughuli za Mkutano Mkuu zitatanguliwa na kuweka Jiwe la Msingi la Majengo ya Ukumbi wa Mikutano na Makao Makuu ya CCM eneo la Medelii katika Manispaa ya Dodoma. Shughuli hii itafanywa na Mwenyekiti wa CCM Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete.

MAANDALIZI YA MKUTANO

Shughuli za Maandalizi ya Mkutano zinaendelea vizuri. Shughuli hizi ni pamoja na uchapaji wa Nyaraka mbalimbali; usafiri wa Wajumbe, Maandalizi ya Ukumbi na huduma nyingine muhimu kwa ajili ya kufanikisha Mkutano huo.

VURUGU ZILIZOTOKEA MBAGALA

Chama cha Mapinduzi kimesikitishwa na matukio yaliyotokea Mbagala, jijini Dar es Salaam, tarehe 11 Oktoba 2012. Chama Cha Mapinduzi kinalaani kitendo cha kukojolewa kwa kitabu kitakatifu cha dini ya Kiislam, yaani Kuran. Vilevile, Chama cha Mapinduzi kinalaani vitendo vya vurugu na kuvamiwa na kuchomwa moto makanisa.

Vitendo vyote hivi havifanani na mila na desturi za Watanzania. Kitendo cha kukojolea kitabu kitakatifu cha Waislamu hakikubaliki. Na kitendo cha kuvamia na kuchoma moto nyumba za ibada za Wakristo na kufanya vurugu pia hakikubaliki. Tanzania ni nchi inayofahamika na kusifika kwa amani na utulivu na kwa umoja na mshikamano wa watu wake wa kabila, rangi na dini zote. Chama Cha Mapinduzi kinawasihi wananchi wawe na subira na uvumilivu yanapotokea matukio kama haya na waviachie vyombo vya dola vifanye kazi yake.

Ni imani ya CCM kwamba vyombo vya dola vitachukua hatua stahiki kwa wote waliohusika na matukio haya. Pia, tunatumaini kwamba hali ya amani na utulivu itarejea Mbagala kama kawaida.

UTEUZI WA MAJINA YA WAGOMBEA NAFASI MBALIMBALI

MKOANI KILIMANJARO


Kamati Kuu pia imefanya uteuzi wa mwisho wa majina ya Wanachama wa CCM walioomba nafasi za Uongozi ndani ya Chama Cha Mapinduzi katika nafasi za Uenyekiti wa CCM Wilaya na Ujumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa nafasi ya Wilaya za Siha na Moshi Vijijini.

Kwa mujibu wa Katiba ya CCM; uteuzi wa mwisho wa nafasi hizi hufanywa na Halmashauri Kuu ya Taifa, lakini Kikao cha tarehe 25/9/2012 kilichofanyika Mjini Dodoma hakikufanya uteuzi wa wagombea wa nafasi hizi katika Wilaya za Siha na Moshi Vijijini. Hivyo, Kikao hicho kilikasimu madaraka yake ya uteuzi kwa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa.

Nafasi za Uongozi zinazogombewa na majina ya walioteuliwa ni kama ifuatavyo:-

(1) Nafasi ya Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Moshi Vijijini

Waliojitokeza kugombea nafasi hii ni 13. Walioteuliwa ni wanne (4) wafuatao:-

(a) Ndugu Shayo Isack EDWARD

(b) Ndugu Masenga John GABRIEL

(c) Ndugu Shao C. GEOFREY

(d) Ndugu Mallya Mathew MARTIN

(2) Nafasi ya Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Siha

Waliojitokeza kugombea nafasi hii ni wanne (4). Walioteuliwa ni wanne (4) wafuatao:-

(a) Ndugu Tawida Nahato BASSO

(b) Ndugu Simon Lekshon MOLLEL

(c) Ndugu Happiness Mathias MUNUO

(d) Ndugu Oscar Jeremiah TEMI

(3) Nafasi ya Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa Wilaya ya Siha

Waliojitokeza kugombea nafasi hii ni saba (7). Walioteuliwa ni wanne (4) wafuatao:-

(a) Ndugu Meijo Loloinyo LAIZER

(b) Ndugu Joha Shabani MTAWAZO

(c) Ndugu Happiness Mathias MUNUO

(d) Ndugu Cosmas Sebastian MUSHI

CCM BLOG