HABARI MPYA

Wednesday, January 23, 2013

CCM KUTUMIA PIA SHEREHE ZA MIAKA 36, KUTATHMINI UCHAGUZI WAKE MKUU ULIOPITA


NA BASHIR NKOROMO, DAR ES SALAAM
PAMOJA na mambo mengine, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimepanga kuzitumia sherehe za miaka 36 ya kuzaliwa kwake, kufanya tathmini ya uchaguzi wake mkuu wa viongozi mbalimbali uliomalizika mwishoni mwa mwaka jana.

Lengo la tathmini hiyo ni kujifunza au kukumbushana kwa kina changamoto zilizojitokeza, hivyo kuitumia fursa hiyo kujipanga vizuri zaidi kwa ajili ya uchaguzi mkuu mwingine wa ndani ya Chama wa mwaka 2017.

Hayo yalisemwa na Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye alipozungumza na waandishi wa habari leo, Januari 21, 2013, katika Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM, jijini Dar es Salaam.

Nape alisema, sherehe za miaka 36 ya kuzaliwa kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM), zitafikia kilele chake Februari 3, 2013, na zitafanyika Kitaifa kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika mjini Kigoma.

Alisema, mgeni rasmi katika sherehe hizo ni Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete na zitahudhuriwa pia na Makamu Wenyeviti wa CCM (Zanzibar) Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein, Makamu Mwenyekiti wa CCM (Bara) Philip Mangula na Wajumbe wote wa Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya Taifa wakiongozwa na Katibu Mkuu, Abdulrahman Kinana.

Nape alisema, uamuzi wa kufanya kilele cha sherehe hizo kuwafanyika Februari 3, 2013 ni kutokana na tarehe yenyewe ya kuzaliwa kwa CCM, ambayo ni Februari 5, 2013 kuwa siku ya kazi, hivyo kutoweza kutoa fursa kwa wanachama kushiriki kwa ufanisi katika sherehe hizo muhimu kwao.

"Sherehe hizi za miaka 36 ya kuzaliwa kwa CCM zinafanyika ikiwa ni takriban miezi miwili tu tokea kumalizika kwa uchaguzi mkuu wa ndani ya Chama na jumuiya zake zote ukamilike Novemba 13, 2012,
Kwa hiyo ni sherehe muafaka kujipongeza na vilevile kuwashukuru wanachama wake kwa kukamilisha kwa ufanisi uchaguzi huo", alisema Nape.

Alisema ili kuwashirikisha wanachama katika ngazi zote, uzinduzi wa sherehe hizo utafanyika kwenye matawi yote, Jumatano Januari 30, 2013, kwa kufanya mikutano ya wanachama wote, nafasi ambayo itatumika kufanya tathmini ya uchaguzi mkuu wa CCM na jumuiya zake wa mwaka 2012 katika ngazi hizo.

Nape alisema Alhamisi Januari 31, 2013 itakuwa ni siku ya Umoja wa Vijana (UVCCM) ambapo wanachama wa jumuiya hiyo watashiriki katika shughuli mbalimbali za kijamii ambazo alisema ni pamoja na usafi wa mazingira na upandaji wa miti.

"Kazi nyingine zitakazofanywa na vijana ni kujadili mafanikio ya UVCCM katika kipindi cha miaka 36 tokea kuzaliwa kwa CCM na Shughuli nyingine itakuwa ni kufanya tathmini ya uchaguzi mkuu wa CCM na jumuiya zake wa mwaka 2012, na mwisho ni kufanyika kwa matamasha mbalimbali ya michezo yatakayowahusisha vijana wote". alisema Nape.

Alisema Februari Mosi, 2013, itakuwa Siku ya Umoja wa Wazazi. Hao watashiriki katika shughuli za kijamii ikiwa ni pamoja na kupanda miti, kushiriki katika ujenzi wa miradi ya maendeleo kama vile ujenzi wa madarasa, zahanati, nyumba za walimu na kadhalika.

Shughuli nyingine itakayofanywa na Wazazi ni kufanya tathmini ya uchaguzi mkuu wa CCM na jumuiya zake wa mwaka 2012, na pia watajadili mafanikio ya jumuiya hiyo yenyewe kwa miaka 36 iliyopita.
Jumamosi Februari 2, 2013 itakuwa siku ya Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT).

Nape aliendelea kueleza kwamba shughuli zitakazofanywa na wanachama hao wa UWT ni kufanya usafi, kupanda miti, kutembelea na kufariji wagonjwa katika hospitali na vituo vya afya, kutembelea vikundi vya uzalishaji mali vya kina mama, kufanya tathmini ya uchaguzi mkuu wa CCM na jumuiya zake wa mwaka 2012 na mwisho ni kujadili mafanikio ya UWT kwa miaka 36 iliyopita.

Siku ya kilele cha sherehe hizo ambazo alisema kaulimbiu yake ni Umoja ni Ushindi kutafanyika Matembezi ya Mshikamano na kwamba wanachama wa CCM na jumuiya zake zote nchini kote ambazo ni UVCCM, Wazazi na UWT watafanya Matembezi ya Mshikamano katika kila tawi kwa muda ambao kila tawi litaona unafaa kwa kuzingatia hali halisi ya mazingira ya eneo husika.

Vilevile itafanyika mikutano ya wanachama wote kwenye matawi, kata, wilaya na mikoa ambayo itatumika kupokea na kujadili maazimio ya Mkutano Mkuu wa CCM uliofanyika tarehe 11 – 13 Novemba, 2012 na utekelezaji wa Mradi wa Awamu ya Tatu wa Kuimarisha Chama.

No comments:

Post a Comment