Na Richard Mwaikenda,Bagamoyo
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimekomba wanafunzi 230 wa Chuo cha Ukutubi na Uhifadhi wa Nyaraka za Serikali (SLADS),waliojiunga na chama hicho wilayani hapa,wakati wa kampeni za ndani za kupanga mikakati ya ushindi wa kishindo katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika mwishoni mwa mwezi huu.
Wanachama hao wapya ambao ni miongoni mwa wanafunzi 500 wa chuo hicho, walikabidhiwa kadi na Mjumbe wa Kamati ya Utekelezaji ya Baraza Kuu la Vijana (UVCCM) Taifa, Ridhiwani Kikwete mjini hapa jana.
Akisoma risala ya wanachama hao, Katibu wa muda wa CCM wa tawi la SLADS, Happy Mgoba, alisema wameamua kuunda tawi hilo ili thamani ya chama hicho itambulike vyuoni.
"Licha ya kazi kubwa, lakini tunapambana vilivyo kuhakikisha thamani ya CCM inatambulika vyuoni,kwani vijana ni Taifa la leo, kesho na kesho kutwa na watakuwa mabalozi wa chama popote watakapokuwa,"alisema Mgoba huku akishangiliwa na wanachama hao wapya.
Mgoba, alitaja mikakati mingine wanayoifanya kukipa nguvu zaidi chama hicho vyuoni kuwa ni;kuwashawishi wanachuo wengine ili wajiunge kwa wingi na chama hicho na kwamba wapo mbioni kuunda shirikisho la wanaCCM la vyuo vikuu vitano vilivyopo wilayani Bagamoyo ambavyo ni, SLADS, Taasisi ya Sanaa Bagamoyo, Chuo cha Uvuvi Mbegani, Chuo cha Uguuzi na Chuo cha Utumishi.
Alitaja baadhi ya changamoto walizonazo kuwa ni;tawi hilo kutokuwa na ofisi,sare za chama,Katiba na ilani za chama hicho.
Ridhiwani, alikipongeza kitendo hicho na kutoa mwito kwa vyuo vingine nchini kuiga mfano huo kwa lengo la kupata vijana wengi wasomi ndani ya chama hicho watakaokuwa tegemeo kubwa katika mustakabali mzima wa maendendeleo ya nchi.
"Msitetereke wala msiogope kujiunga na CCM, kwani ukiwa CCM mambo yatakwenda vizuri. Hamtapata majuto bali mtapata faraja zaidi.Tutawashirikisha kwa kila kitu kwani maandalizi ya kuongoza Serikali linaanzia kwa wasomi makada,"alimalizia kusema Ridhiwani.
Awali Ridhiwani na kikosi chake, walipokelewa kwa vifijo na mbwembwe za pikipiki zilizopamba msafara wake na kuufanya mji wa Bagamoyo kuzizima kwa muda hali iliyoashiria kuwa kweli mcheza kwao hutuzwa.Ridhiwani ambaye ni mtoto wa Rais Kikwete ni mzaliwa wa Wilaya ya Bagamoyo
No comments:
Post a Comment